Hongera kwa blog yako nzuri inabariki pia.

Mimi ni mama wa umri wa miaka 30 sasa tatizo langu ni hili naomba unishauri binafsi, ikiwezekana na wasomaji wako wa blog waweze kunishauri. Pia naombeni maombi yenu pia sababu nahisi nakufa taratibu kabla ya siku yangu kufika. Naomba Email yangu uiweka kapuni.

Nimeolewa na nimeokoka kwelikweli. Mwaka wa 6 sasa katika ndoa sijapata mtoto, sijawahi kupata mimba wala kuhisi dalili hizo. Nimezunguka, nimetibiwa, nimepimwa na kila njia kwa kadri ya uwezo wangu lakini hola. Chakushangaza ni kwamba kila nitakavyopimwa na kutibiwa vipimo vyangu pamoja na mwanaume vinaonesha ni mzima ila madaktari wanajaribu kunipa dawa labda za kuharakisha na kadharika.

Nimeshaombewa dada nimeshajiombea na marafiki ndugu na jamaa lakini wapi tatizo lipo pale pale. Siku moja nikajipa ujasiri nikasema kwakuwa napenda watoto sina tatizo ila Mungu hajanifungulia njia nikachukue mtoto mchanga wa kumu-adapt ili awe kama wangu nimlee kwa mapenzi yote yaani huwezi kuamini mume wangu alinibadilikia aligomba akaanza kunituhumu kuwa huenda namu-enjoy labda najua tatizo langu au ni mgumba mimi yaani sikuamini ninachokisikia aisee isitoshe yeye ana watoto wake wawili amewazaa na mwanamke mwingine kabla sijaolewa nae. Sasa nimekaa najiuliza hivi huyu shetani ni wa aina gani ambaye asikii maombi au Mungu anataka kunipa watoto wa uzeeni kama alivyofanya kwa Sara na Elizabeth kwenye biblia. Ninamawazo yasiyoisha nilikuwa napenda sana watoto hivyo nilikuwa nakusanya watoto wa majirani nashinda nao kila wikiendi n.k kwa sasa sijui nimeathirika kisaikolojia sitaki tena hata kuona mtoto wa mtu mbele ya macho yangu kiufupi nawachukia. Muda wote nipo ndani peke yangu ata nikiwa ofisini ni peke yangu siwezi kukaa dk tano bila kutoa machozi. Imefika wakati hata rafiki zangu nikiwa nao wanaongelea stori za watoto wao n.k. ninapochangia nitaambiwa subiri kwanza uzae wako ili uone uchungu wa mtoto. Ni mtoto wa kwanza katika familia yetu na nina wadogo wawili wa kike na wa kiume na wote wameshapata watoto ila mimi sijapata hadi sasa.

Nimekaa hapa na mawazo tele ambapo naona hayana majibu nikajipangia mwenyewe hadi tarehe 28/2/2014 kama nitaendelea kuwa hivi na gharama zote hizi  za matibabu zilizotumia mpaka nimebaki na - kwenye akaunti yangu pasipo mafanikio basi nijiuwe tu ili nimalize stori za utasa zinazonizunguka. Na pia nimewaza wachungaji wote hawa walioniombe pamoja na Mchungaji wangu kiongozi ambaye yupo bega kwa bega na mimi kwa ushauri na maombi sifanikiwi  Je ni kosa gani kubwa ambalo nilimkosea Mungu mpaka akaweka alama katika maisha yangu isiyopungua wala kufutika.

Siku moja mwenyewe umetoa ushuhuda wa maombi ya kujiambatanisha basi siku hizi kila ninapokaa na mjamzito au ninapohudhuria hospitali kwa ajili ya ushauri wa kidaktari najiambatanisha na wanawake wajawazito mpaka najiona chizi saa nyingine. Ila nikiwa peke yangu ndio najikumbushia ahadi yangu ya kujiuwa ifikapo tarehe  hiyo 28/2 nimekaa nalo mpaka naona tarehe hizo zinafika naombeni mnishauri wapendwa je hayo ndiyo yale majaribu tunayoyasoma kama ya Ayubu au ni kitu gani ninachokutana nacho katika maisha yangu.

Asante na Mungu akubariki